DAWA GANI YA MENO NI SAHIHI
Dawa ya meno ni bidhaa ya kusafisha meno ambayo hutumiwa kwa pamoja na mswaki ili kusaidia katika kusafisha meno, kudumisha afya ya kinywa, na kuzuia matatizo kama vile kuoza kwa meno na ugonjwa wa fizi.
Vitu muhimu vya kuzingatia kabla hujanunua dawa ya meno
Ikiwa ni kweli kwamba dawa za meno zipo za aina nyingi lakini lengo kuu la dawa hizi linabaki kuwa lile lile – kukukinga na magonjwa ya fizi na meno. Hivyo basi, wanasayansi wamebaini vitu muhimu ili dawa yako unayotumia mbali na kuangalia ladha, rangi, muundo au harufu ya dawa ambayo ungependezwa nayo zaidi.
Ni vyema kuvifahamu vitu hivi ili hata kabla hujaangalia vionjo vingine basi hivi ndivyo viwe vya kwanza kuzingatia wakati wa kununua dawa yako ya meno.
1.Madini ya floridi
Madini ya floridi hukinga meno na magonjwa kwa kufanya meno kuwa magumu zaidi na kuzuia kuharibiwa na bakteria. Madini haya huunganika na sehemu ya nje ya jino (enamel) na kutengeneza muundo uitwao fluoroapatite ambao huongeza uimara zaidi wa jino.
Kuna aina tatu kuu za madini haya ambayo utakuta katika dawa yako ya meno. Kufahamu hizi itakusaidia ujue ni aina gani ya dawa ya meno utahitaji kulingana na mahitaji yako kwa wakati huo.
Aina ya kwanza ni Sodium fluoride, ya pili ni Sodium monofluorophosphate.
Hizi hufanya kazi sawa kwa kuongeza tu uimara wa meno na kukinga kutoboka kwa meno yako.
Kwa kawaida kabisa, madini ya floridi ya aina hizi mbili huunda dawa ya kukubalika kwa matumizi ya kila siku na yenye kukidhi vigezo vya kuimarisha meno (standard toothpaste) ili kuzuia uharibifu wa meno yako. Unaweza kutumia dawa ya meno yenye aina hizi ya floridi ikiwa huna tatizo lingine lolote katika kinywa chako.
Aina ya mwisho ni stannous fluoride.
Aina hii ya madini ya floridi, mbali na kwamba huzuia kutoboka kwa meno na kuimarisha meno yako, yenyewe ina faida za ziada kama vile kutibu magonjwa ya fizi kama kutokwa na damu au fizi kuvimba (gingivitis), unyeti wa meno (tooth sensitivity), huzuia mmomonyoko wa meno kwa asidi kupitia bakteria na huuwa bakteria wanaoharibu meno.
Hivyo unaweza kutafuta dawa ya meno yenye madini haya ya floridi kulingana na hali yako ya kinywa.
Kiwango gani cha floridi ni sahihi katika dawa yako ya meno ?
Hutegemeana na umri wa mtu.
Kuanzia umri wa miaka 6 na zaidi hutumia dawa ya meno yenye kiwango cha madini ya floridi 1400-1500ppm.(Dawa maalumu ya watu wazima)
Watoto chini ya miaka 6 hutumia kiwango cha 500ppm mpaka 1000ppm. .(Dawa maalumu ya watoto)
Kumbuka taarifa zote hizi unazipata kwenye boksi la dawa ya meno kabla ya kununua
2.Madini ya Potassium nitrate
Haya madini husaidia kuondoa wepesi kuhisi (sensitivity) katika meno yako.Wepesi kuhisi wa meno ni ile hali ya kuhisi maumivu kwenye meno ambayo hukaa kwa muda mfupi baada ya aidha kupiga mswaki, kunywa, kula, au hata pale upepo unapopita katika kinywa chako.
Hali hii hutokana na ile sehemu ngumu ya nje ya jino kulika sana (enamel erosion) hivyo jino kuwa wazi au mzizi wa jino unapokuwa nje kutokana na fizi kushuka chini zaidi ya eneo lake la kwanza ambapo hufunika jino.
Hivyo basi, kwa mtu mwenye tatizo hili, ni vyema kununua dawa yenye madini haya ili kusaidia tatizo hilo. Taarifa za madini haya hupatikana pia katika sehemu ya viungo hai, katika boksi lako la dawa ya meno.
3.Uwezo wa Kusafisha na Kung'arisha:
Chagua dawa ya meno yenye viambato vya kusafisha kama vile abrasive ambayo husaidia kuondoa madoa ya juu ya meno bila kuharibu enamel.
Ikiwa unataka meno yako yaonekane meupe zaidi, unaweza kuzingatia dawa za meno zenye viambato vya kung'arisha meno. Lakini kuwa mwangalifu kwani baadhi zinaweza kuwa na abrasive kali ambayo inaweza kuharibu meno ikiwa itatumika kupita kiasi..
Matumizi sahihi ya dawa ya meno.
Inashauriwa kutumia kiasi kidogo cha dawa ya meno;
Watu wazima kiasi cha ukubwa wa brashi ya mswaki ni cha kutosha
Watoto wanapaswa kutumia kiasi kidogo zaidi sawa na ukubwa wa punji ya harage).
Dawa ya meno inapaswa kutumika angalau mara mbili kwa siku, asubuhi baada ya chai na jioni baada ya chakula kabla ya kulala.
Faida za Kutumia Dawa ya Meno:
Kuzuia kuoza kwa meno: Floridi katika dawa ya meno husaidia kuimarisha meno dhidi ya mashambulizi ya asidi inayosababishwa na chakula.
Kung'arisha meno: Abrasives husaidia kuondoa madoa kwenye meno na kuyafanya yaonekane meupe zaidi.
Kuzuia magonjwa ya fizi: Baadhi ya dawa za meno zina viambato vinavyosaidia kupambana na vijidudu vinavyosababisha matatizo ya fizi.
Kutoa harufu nzuri kinywani: viambata ladha (flavouring agents)husaidia kupunguza harufu mbaya ya kinywa na kuweka pumzi safi.
Hitimisho
Kwa ujumla, uchaguzi wa dawa ya meno unapaswa kuzingatia mahitaji ya mtu binafsi na ushauri wa daktari wa meno kwa ajili ya kulinda afya ya kinywa na meno