MENO KUVUNJIKA/KUPASUKA
Ni jambo la kawaida sana kuskia mtu anasema jino langu limemeguka,limepasuka au ni kipande. Jino kupasuka ni ile hali ya sehemu ya nje ya jino (enamel) kupata nyufa na kudhoofika kupelekea kumeguka.Hii inaweza kusababishwa na mambo mengi lakini habari njema ni kwamba matibabu mbalimbali yapo kulingana na hali ya jino lenyewe.Kwa takwimu sisizo rasmi meno ya mbele ya kung’atia (incisors) na meno ya nyuma ya kutafunia (Molars) yanatabia ya kupasuka Zaidi ukilinganisha na mengine.
Sababu za Kuvunjika au Kupasuka kwa Meno:
✓Ajali: Mapigo kwenye mdomo yanayoweza kusababishwa na ajali za michezo, kugongwa au kuanguka.
✓Tabia hatarishi:kutafuna vitu vigumu kama barafu,karanga au penseli kunaweza kusababisha meno kuvunjika.Lakini pia matumizi ya meno kufungulia vinywaji kama bia na soda inaweza kupelekea jino kuvunjika.
✓Kuuma kwa nguvu sana:kubana meno kwa nguvu sana (bruxism) kunaweza kusababisha jino kusagika,ufa au kupasuka kwa jino.
✓Meno yaliyooza/kutoboka:Uozo wa meno (cavity) unaweza kudhoofisha meno, na hivyo kuwa na uwezekano mkubwa wa kupasuka au kuvunjika.
✓Umri mkubwa:uzee hupelekea meno kudhoofu hivyo inakua rahisi kwa mzee jino kupasuka kuliko kijana
✓Mabadiliko ya joto: Unywaji wa vinywaji vya moto kisha baridi (au kinyume chake) unaweza kufanya meno kupasuka kwa mabadiliko ghafla ya joto.
Dalili za Kuvunjika au Kupasuka kwa Meno:
~Maumivu makali: hasa wakati wa kuuma au kutafuna chakula.
~Ugonjwa wa fizi: kuvimba kwa fizi karibu na jino lililovunjika.
~Meno kupata hisia kali (hypersensitivity): Meno kuwa na hisia kali kwa vinywaji au vyakula vya moto na baridi,vyakula vyenye tindikali.
~Uonekano wa ufa: Ufa unaweza kuonekana kwenye jino husika lililovunjika.Mara nyingi pia hutokea kama mstari wa rangi nyeusi.
~Jino kuwa na ncha kali: Kipande cha jino kilichovunjika kinaweza kuwa na ncha kali na kudhuru ulimi au mashavu.
Matibabu ya Kuvunjika au Kupasuka kwa Meno:
✓Kujaza/kuziba jino (Filling): Ikiwa ufa ni mdogo, daktari wa meno anaweza kutumia vifaa maalum na dawa kama Helioseal kujaza eneo lililoharibika au ufa unaoanza.
✓Taji/kofia ya bandia(Crown): Jino lina sehemu ya juu(crown) na sehemu ya mzizi. Kama sehemu ya juu imevunjika kwa kiwango kikubwa,taji la bandia linaweza kuwekwa sehemu ya juu ili kulinda na kuimarisha jino.
✓Kuweka nira (Veneers): Kwa meno ya mbele yaliyopasuka, nira za porcelain au resin zinaweza kuwekwa kufunika ufa au sehemu iliobaki ya jino.
✓Matibabu ya mizizi (Root Canal): Ikiwa ufa au mpasuko unafikia mizizi ya jino kuchagiza maumivu makali au kupelekea jipu la jino, matibabu ya mizizi yanaweza kuhitajika ili kuondoa maumivu na kuokoa jino.
✓Kung'oa jino: Mwisho kabisa ikiwa jino limeharibika sana kiasi cha kutoweza kurekebishwa, kung'oa linaweza kuwa suluhisho.
Namna ya Kujiepusha na Kuvunjika meno
Epuka kutafuna vitu vigumu: Vitu kama barafu, kalamu, na karanga ngumu vinaweza kuharibu meno.
Vaa vifaa vya ulinzi wakati wa michezo: Wakati wa michezo ya hatari kama mpira wa miguu au ndondi, tumia kinga ya mdomo(mouth guard) ili kulinda meno.
Ondoa mazoea ya kung'ata meno (Bruxism): Kama unasaga meno wakati wa kulala, zungumza na daktari wa meno kuhusu kutumia kinga ya meno usiku (night guard).
Tumia meno kwa kazi zinazofaa: Usitumie meno kufungua vinywaji,vifungashio au kuvuta vitu.
Punguza vyakula na vinywaji vyenye sukari nyingi: Kuzuia kuoza kwa meno (cavities) ambayo huongeza hatari ya meno kuvunjika.
Kufanya uchunguzi wa mara kwa mara kunaweza kusaidia kugundua matatizo ya meno mapema na kuyatibu kabla ya kuharibika Zaidi.