JINO LILILOTOBOKA NI KARAHA KWA MTANZANIA
JINO LILILOTOBOKA NI KARAHA KWA MTANZANIA
Oct. 25, 2024

KUOZA AU KUTOBOKA  KWA MENO
Kuoza, kutoboka ama kuharibika kwa meno (Kitaalamu hujulikana Dental Caries), ni tatizo ambalo husababisha meno kumomonyoka na kutengeneza shimo ama kubadilika rangi kuwa kama rangi ya chaki, kijani kibichi hadi nyeusi.
 
Hali hii hutokana na shughuli za vimelea vya Bakteria na huanza taratibu na kuongezeka siku hadi siku na huweza kuathiri jino lolote lile, lakini hujitokeza sana kwenye meno ya nyuma (Magego). 
Hali hii inaweza kutokea kwa mtu yeyote na kwa umri wowote, isipokuwa watoto ambao hawajaota meno

Nini kinasababisha meno kuoza?
Kinywani kuna Bakteria wasiokuwa na madhara. Bakeria hawa humeng’enya mabaki ya vyakula mdomoni haswa vyakula na vinywaji vyenye sukari nyingi na matokeo yake huzalisha tindikali (asidi) kwa wingi kinywani. Tindikali hii huyeyusha na kumomonyoa na kuharibu madini yanayopatikana kwenye sehemu ya nje ya jino inayoitwa “Enamel” na hatimaye kutengeneza uozo (shimo) kwenye meno.

Usafi hafifu wa kinywa na meno na kusababisha mabaki ya chakula kukaa muda mrefu kinywani.

Upungufu wa mate mdomoni, kutokana na ugonjwa wa kisukari, Sjogren’s Syndrome kupumua kwa mdomo kwa muda mrefu na upungufu wa maji mwilini kwa muda mrefu ama kutokunywa maji ya kutosha.

Dalili za meno kuoza
-Meno kupata ganzi.
-Maumivu ya meno wakati wa kula vyakula vya baridi ama vya moto, na wakati wa usiku hali ambayo inaweza kusababisha ukose usingizi.
-Jino (Meno) kuwa na shimo.
-Kuwa na rangi nyeusi kwenye jino (meno) husika.

Matibabu kwa jino lililotoboka.
Watu wengi hukimbilia kung’oa meno yaliyotoboka. Lakini ukweli ni kwamba kuna njia nyingi ambazo zinaweza kutibu jino lililotoboka kabla halijafikia hatua ya kung’oa. 
Baadhi ya njia hizo ni pamoja na:
Kuziba kwa dawa ya muda mfupi (Temporary filling).
Kuziba kwa dawa ya muda mrefu (Parmanent filling).
Kutibu mzizi wa jino (Root Canal Treatment).
Kukata ncha ya mzizi wa jino (Apicectomy).
Kuondoa kiini cha jino (Pulpotomy).
Kung’oa jino lililoharibika vibaya sana.

Nifanye nini kuzuia meno kuoza? 
Safisha kinywa na meno yako kwa mswaki na dawa ya meno yenye madini ya floridi angalau mara mbili kwa siku (asubuhi baada ya chai na baada ya chakula cha usiku kabla ya kulala). CERVITEC F na FLUORO PROTECTOR S ni dawa zenye madini mengi ya floridi ambayo huimarisha na kuweka ulinzi imara kwenye jino na hatimaye kuondoa kabisa athari za Tindikali (asidi) inayoweza kuharibu meno.  

Epuka matumizi ya vyakula na vinywaji vyenye sukari nyingi kama Biskuti, Pipi na Juisi. Pia unashauriwa kusafisha kinywa na meno kila baada ya kutumia vyakula na vinywaji hivyo.

Tumia vyakula vyenye virutubishi kwa wingi kama vile Maziwa, Mbogamboga za kijani kama vile Spinachi, Matunda, Karanga,Mafuta ya nazi na Parachichi.Epuka vyakula vilivyosindikwa.

Fanya uchunguzi na kupata ushauri juu ya Afya ya Kinywa na Meno kwa daktari wako angalau mara mbili kwa mwaka

WhatsApp