HARUFU MBAYA MDOMONI (HALITOSIS)
Harufu mbaya, kwa kitaalamu huitwa Halitosis, ni tatizo ambalo huathiri watu kulingana na kile wanachokula, namna wananvyotunza afya ya vinywa na meno yao. Lakini pia huweza kusababishwa na changamoto zingine mbalimbali za kiafya, haswa katika mfumo wa hewa na mmeng’enyo wa chakula.
Visababishi vya harufu mbaya mdomoni
Kutokuzingatia usafi wa kinywa; Hii husababisha mabaki ya chakula kujilimbikiza kwenye meno na kuchochea uzalianaji wa bakteria na kusababisha harufu mbaya.
Maambukizi mdomoni kama vile ugonjwa wa fizi, kutoboka kwa meno na vidonda mdomoni (Tonsilitis).
Matumizi ya tumbaku:Kutafuna tumbaku na kuvuta sigara huongeza athari ya ugonjwa wa fizi na kusababisha harufu mbaya mdomoni.
Matumizi wa vyakula vyenye harufu kama vile vitunguu na vitunguu swaumu,vyakula vya sukari,kahawa na jibini.
Maswala ya mmeng’enyo wa chakula kama vile kuvimbiwa na magonjwa ya tumbo na utumbo.
Upungufu wa maji mwilini, na upungufu wa mate mdomoni (Mdomo kuwa mkavu kwa muda mrefu).
Magonjwa ya mfumo wa hewa yanayoathiri koo la hewa na mapafu.
Jinsi ya kuzuia harufu (pumzi mbaya) mdomoni
Safisha kinywa na Meno yako kwa kupiga mswaki mara mbili kwa siku, asubuhi baada ya chai na baada ya chakula cha jioni kwa kutumia mswaki laini na dawa ya meno sahihi.
Safisha ulimi kwa mswaki maalum au kipakaza ulimi (tongue scrapper) angalau mara moja kwa siku.
Acha kuvuta sigara na epuka matumizi ya tumbaku
Kunywa maji mengi ili kuhakikisha kinywa kina unyevu mwingi na mate ya kutosha
Tafuna Peremende isiyokuwa na sukari au “Xylitol gum” ili kuongeza uzalishaji mate mdomoni kwa ajili kutunza usafi wa kinywa.
Kama tatizo linasababishwa na ugonjwa kwenye mfumo wa upumuaji au umeng’enyaji wa chakula jitahidi kupata matibabu.
Mtembelee daktari wako wa kinywa na meno kwa ajili ya uchunguzi na ushauri zaidi.